Resources » News and Events

WAZIRI DK.KIGWANGALLA AZINDUA BODI YA USHAURI YA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA ,ATOA PONGEZI

Wajumbe wa Bodi (Waliokaa Kushoto), Prof. Dos Santos Silayo , Br. Jenerali Mkeremy, Mh. Dr, Khamis Kigwangalla

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk.Hamisi Kigwangalla amesema kuwa tangu kuazishwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu( TFS) ambao umefikisha miaka minane sasa yameshuhudiwa mafanikio ya  kuridhisha.

Mafanikio hayo yameonekana pia kupitia ya taarifa ya Bodi (II) ya Tathmini ya Utendaji wa Wakala (2014/15- 2017/18) katika usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki huku pia ikionesha Wakala umejenga misingi ya kitaasisi ikiwemo kuimarisha mifumo ya kiutendaji; kuongeza kasi ya upandaji miti kwenye mashamba na kuongoa maeneo yaliyoharibika.

Dk.Kigwangalla ameyasema hayo leo Machi 9,2019 wakati akizindua Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).Uzinduzi wa bodi hiyo umefanyika leo Machi 9 jijini Mwanza na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.

Ametumia nafasi hiyo kufafanua kwa ukubwa wa eneo la misitu lililonalo kama taifa na mtawanyiko wa bionuai yake bado mchango wa sekta kwenye pato la Taifa ni mdogo. Pamoja na changamoto za kukokotoa mchango huo bado kuna wajibu wa kuonesha ile michango ya moja kwa moja kwa kubuni matumizi ya misitu yaliyo endelevu.

Hivyo amesema bodi hiyo haina budi kubuni mikakati itakayowezesha mashamba ya miti kuongezeka na kusimamiwa kwa njia endelevu na kukuza na kuendeleza utalii kwenye hifadhi za misitu ya mazingira asilia. 

"Vile vile kuwa na mikakati thabiti ya kukuza uchumi wa viwanda kwa kupitia utendaji wa Wakala na ushirikiano na Sekta binafsi au Wananchi, hivyo kutekeleza dhana ya mahusiano ya kibiashara baina ya Serikali-Sekta binafsi (PPP)," amesema Dk.Kigwangalla.

Pia ameitaka bodi hiyo ya ushauri itatekeleza wajibu wake ikiwemo kusimamia sekta ndogo ya nyuki na kwamba  upo ushahidi wa kimazingira nchi yetu inaweza kufaidika sana na rasilimali nyuki. Kwanza kwa kupata mazao yake kama asali, nta na mengine kibishara

"Pia kuitumia kama mfumo wa kibailogia wa kuzuia wanyama waharibifu wa mazao na wasumbufu kwa wananchi. Nimeshaelekeza juhudi za makusudi ziwekwe na taasisi mbalimbali za uhifadhi katika wizara katika kuongeza kasi ya ufugaji na uzalishaji wa mazao ya nyuki.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dr. Khamis Kigwangalla akiongea wakati wa Uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)

Ameongeza kuwa hilo ni eneo ambalo anaihitaji bodi hiyo kuendelea kulisimamia na kushauri kwa umakini muda wote na kuongeza maagizo  kama haya pia ameyatoa kwa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF).

"Ni matumaini yangu mtashirikiana kufanikisha mabadiliko makubwa katika sekta hiyo.Nyuki wakitumika vizuri wataongeza kipato kwa jamii zinazozunguka misitu na hivyo kupungua utegemezi wao kwenye misitu ambao mara  nyingi unapelekea uharibifu mkubwa," amesema.

Dk.Kigwangalla amesema jambo lingine muhimu kwa bodi inapaswa  kulifahamu ni kwamba wizara ya Maliasili na Utalii imebadili mfumo wake wa usimamizi wa maliasili toka ule wa kiraia kwenda mfumo wa kijeshi (Paramilitary).

 Kuhusu TFS Dk.Kigwangalla amesema imekuwa mstari wa mbele kwenda na mabadiliko hayo kwa kuanza kutekeleza mafunzo ya watumishi katika ngazi mbalimbali. Kinachosubiriwa sasa ni kupitisha mabadiliko ya muundo wao wa utumishi utakaotambua mabadiliko ya vyeo na majukumu ya kila siku.

Aidha, amesema wizara inaendelea kukamisha sheria ya Jeshi Usu pamoja na mapitio ya nyenzo za utendaji kama General Oders. Hivyo, bodi hiyo inapaswa kuendelea kuendelea kusimamia mabadiliko ya muundo huo na baadaye kusimamia utendaji wa mfumo mpya ili kuleta ufanisi unao

Kuhusu kuzinduliwa kwa  bodi hiyo ya Ushauri ya TFS, amewapongeza wote walioteuliwa katika bodi hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Brigedia  Generali Mbaraka Mkeremy.

"Natambua kuwa mna majukumu mengine katika kujenga Taifa letu lakini kwa kutambua umuhimu wa sekta ya misitu na nyuki mmekubali jukumu la kuishauri Wizara kuhusu utendaji wa TFS katika masuala yote yanahusiana na usimamizi na uendelezaji wa sekta ya misitu na nyuki nchini," amesema.

Ameongeza ana imani kuwa uzoefu na umahiri wao  utaongeza tija na kuboresha utendaji wa Wakala na uhifadhi kwa ujumla na kwamba

Tanzania imebahatika kuwa na rasilimali za misitu na nyuki ambazo ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya nchi.

Dk.Kigwangalla amesema sekta ya misitu ni msingi katika ukuaji wa sekta nyingine muhimu zikiwemo maji, kilimo, utalii, mifugo, viwanda na nishati kwa sababu ya uwezo wake wa kuhimilisha mifumo ekologia.  Hivyo, hatuna budi kuhakikisha rasilimali hizi zinalindwa na kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

"Takwimu tulizonazo zinaonesha kuwa rasilimali za misitu nchini zinakadiriwa kuwa takribani hekta milioni 48.1 sawa na asilimia 55 za eneo la Tanzania Bara. Kati ya eneo hilo la misitu, Wakala unasimamia rasilimali za misitu zenye ukubwa wa eneo la hekta milioni 16.65 ambazo ni sawa na asilimia 34 ya eneo lote la misitu la Tanzania.

Waziri akimkabidhi Mwenyekiti mpya wa Bodi ya TFS Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremy vitendea kazi tayari kwa kuanza kutekeleza majukumu yake

" Kulingana na takwimu hizo, ni dhahiri kuwa Wakala unasimamia kisheria takribani theluthi moja tu ya eneo lenye misitu na theluthi mbili nyingine zinasimamiwa kisheria na wadau wengine wakiwemo Serikali Serikali za Mitaa zikiwemo za vijiji na halmashauri za wilaya pamoja na ile ya watu au taasisi binafsi. Kwa kuangalia mfumo huo wa usimamizi ni dhahiri changamoto za usimamizi ni kubwa.

"Hivyo nitoe mwito kwa bodi kuendelea kusimamia mabadiliko ya mfumo wa usimamizi utakaopelekea kuwa na mamlaka moja. Mamlaka hiyo itaweza kuyafanyia kazi kwa malengo na vipaumbele vya sekta na kuondoa migongano ya utendaji," amesema.

Amesema Serikali ilianzisha Wakala (TFS) mwaka 2010 ili kuhakikisha uwepo wa usimamizi madhubuti, wenye ufanisi na tija wa rasilimali za misitu na nyuki zilizo chini ya Serikali Kuu; kuongeza thamani ya mazao ya misitu na nyuki na kutoa huduma bora kwa umma kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa umma.

Amesema kiutendaji Wakala unatekeleza majukumu ya iliyokuwa Idara ya Misitu na Nyuki isipokuwa utungaji wa sera, sheria na programu za sekta za misitu na nyuki.