Resources » News and Events

Utiliaji Saini Mkataba wa Ushirikiano wa Matumizi bora ya Ardhi kati ya TFS na NLUPC

TAARIFA YA MTENDAJI MKUU WA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA (TFS)

PROF. DOS SANTOS SILAYO KATIKA TUKIO LA KUTILIANA SAINI MKATABA WA USHIRIKIANO NA TUME YA TAIFA YA MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI (NLUPC) KATIKA KUANDAA MIPANGO SHIRIKISHI YA MATUMIZI BORA YA ARDHI YA VIJIJI VINAVYOZUNGUKA HIFADHI ZA MISITU NCHINI

31 JANUARI, 2019

 1. Mkurugenzi Mkuu, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Dr. Stephen Nindi
 2. Wakurugenzi wa Idara mbalimbali wa Tume
 3. Wakurugenzi wa Idara toka TFS
 4. Watumishi na Wataalam wote mliopo toka taasisi zetu mbili,
 5. Wageni waalikwa
 6. Ndugu Wanahabari,
 7. Mabibi na Mabwana,

Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kutuwezesha kuwa mahali hapa leo. Aidha nikushukuru Dr. Nindi Mkurugenzi Mkuu Tume pamoja na timu yako kwa kutenga muda ili tuweze kukamilisha sehemu ya mazungumzo yaliyopelekea makubaliano ya taasisi zetu mbili katika kutekeleza kazi ya kupanga ardhi kwenye baadhi ya vijiji.

Mtakumbuka mazungumzo na mipango ya kutekeleza jambo hili yalianza tangu mwezi August 2018 ambapo tuliweza kuanza utekelezaji Mwezi December 2018. Tunapokutana leo tunafuraha kwamba kazi hii imeanza na tumepata fursa ya kujifunza mambo mengi katika kuitekeleza.

Ndugu zangu

Kama mnavyofahamu nchi yetu imejaliwa baraka ya kuwa na eneo kubwa lenye uoto mzuri wa misitu ya ekologia mbalimbali. Misitu hii imegawanyika katika ile iliyohifadhiwa na ile ambayo haijahifadhiwa. Aidha, kati ya iliyohifadhiwa ipo inayosimamiwa na serikali kuu na ile iliyokatika usimamizi wa mamlaka za serikali za mitaa. Hii inajumuiya iliyo chini ya halmashauri za wilaya na ile misitu ya vijiji.

Ni ukweli usiopingika kuwa Misitu hii na sekta ya Maliasili kwa ujumla zinakabiliwa na changamoto kubwa katika uhifadhi. Hii inatokana na kubadilika kwa mazingira ya kazi na pamoja na mifumo ya kihalifu. Katika kupambana na kutatua changamoto hizi serikali kupitia wakala imeendelea kuweka jitihada mbalimbali kukabili hali hiyo. Moja ya jitihada hizo ni kusaidia wananchi kupanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyao.

Wakala unaamini kuwa kwa kusaidia wananchi kupanga matumizi sahihi ya ardhi yao kutapunguza muingiliano wa shughuli za kijamii na kiuchumi na hivyo kuondoa migogoro miongoni mwa jamii. Aidha, mipango bora itawafanya wananchi wapunguze kilimo cha kuhama hama ambacho kwa sehemu kubwa huchangia sana katika kupunguza maeneo ya misitu.

Hivyo, katika kutekeleza suala hili TFS inashirikiana Tume ya Matumizi ya Ardhi na mamlaka nyingine za serikali pamoja na wananchi kuhakikisha vijiji lengwa vinapanga ardhi yao. Lakini lengo sio kupanga tu bali pia muhimu zaidi ni kuheshimu mipango hiyo. Kila mwananchi anao wajibu wa kuheshimu mipango inayowekwa.

Hii sio mara ya kwanza kwa TFS kutekeleza mpango. Kwa nyakati mbalimbali TFS kwa kushirikiana na mashirika mengine ya uhifadhi ya Serikali na asasi zisizo za kiserikali imetekeleza miradi ya namna hii. Lakini utekelezaji wa sasa unafanyika kwa ukubwa zaidi na katika mpango ambao ni endelevu. Kwa kuanzia mwaka huu wa fedha tunatarajia kutumia zaidi ya shilingi 1.5 bilioni kutengeneza mipango ya vijiji takribani 100 katika maeneo mbalimbali nchini.

Mradi huu unategemewa kufanikiwa zaidi hususani katika kutekeleza maelekezo ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Dr. John Magufuli ya kufanya mapitio ya maeneo ya hifadhi na kuvitenga vijiji vilivyokwishaanzishwa kwenye hifadhi hizo. Baada ya utambuzi huu vijiji hivyo pia vitafadika na mradi kama huu na hivyo kuwapa fursa wananchi kupanga ardhi na kuhakikisha inatumika vizuri kwa maendeleo endelevu.

Ndugu zangu,

Pamoja na kupanga ardhi katika vijiji vyetu TFS inafanya jitihada kadhaa pia kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za serikali kutatua changamoto za uharibifu wa misitu yetu yetu. Jitihada hizo ni pamoja na;

 1. Kuongeza maeneo ya hifadhi

Jitihada zinaendelea katika maeneo mbalimbali nchini kuhifadhi misitu ambayo haikuhifadhi hapo kabla.

 1. Kupandisha hadhi misitu

TFS inatarajia kupandisha hadhi misitu 5 mwaka huu kuwa Hifadhi za mazingira Asilia ili kulinda zaidi baionuai inayopatikana katika misitu hiyo. Lakini pia kuiwezesha itumike kwa shughuli za utalii.

 1. Utatuzi wa migogoro

Kama mnavyofahamu ni kwamba uharibifu wa misitu ni mkubwa hasa maeneo ambayo vijiji vimeanzishwa ndani ya misitu au maeneo ambayo mipaka ya vijiji au misitu haijulikani vizuri. Hivyo, TFS itaendelea kutatua migogoro ya mipaka kwa kusaidia maandalizi ya mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa vijiji vinavyozunguka misitu ya Hifadhi. Aidha TFS itaendelea kusaidia vijiji kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama maji, mipango ya ardhi, shule nk.

 1. Upandaji miti

TFS imekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuhakikisha miti inapandwa ili kuhuisha ardhi nchini. Tutaendelea kukuza na kugawa miche kwa wananchi pamoja na kuanzisha mashamba mapya ya miti maeneo mbalimbali.

 1. Ununuzi wa vifaa

Vifaa mbalimbali vinanunuliwa kusaidia usimamizi wa rasilimali za misitu nchini. Vifaa hivi vinajumuisha Mitambo, Boti, Magari na Pikipiki. Kwa mwaka 2018 pekee, jumla ya magari 35 yatanunuliwa. Mwaka huu wa fedha mitambo na magari mapya 30 yatanunuliwa.

 1. Kupunguza matumizi ya nishati ya mimea

Matumizi ya Mkaa na Kuni yanatishia sana ustawi wa misitu yetu. Matumizi yake yanatokana na ukweli kwamba hakuna nishati mbadala inayoweza kumudu jamii kubwa na pia usambazi wa hizi zilizopo kama Gas bado ni kwa kiasi kidogo. TFS inaratibu wizara 5 na taasisi za serikali 4 pamoja na sekta binafsi katika kutatua tatizo hili. Tayari Utumishi na Utawala bora wametoa ‘deduction code’ kwa kampuni za Gas ili watumishi wa serikali waweze kukopeshwa Gas na vifaa vyake toka kwenye mishahara. Aidha, TFS inashirikiana na kampuni ya KopaGAS kutafuta fedha kueneza technology ya kuuza gas rejareja kwa mfumo ‘Lipa Unavyotumia – LUKU’. Hii ni pamoja na kusadia sekta binafsi kuzalisha mkaa mbadala (Briquettes)…nk.

 1. Matumizi ya mifumo ya kisayansi na technology

Kutumia mifumo ya kisayansi na technology katika kuratibu shughuli za usimamizi. Hivyo matumizi ya Drones (Ndege zisizo na rubani)  na Satelite ni kipaumbele cha Wakala. Tayari matumizi ya Drones yameanza katika kusimamia misitu ya mikoko na tumeanza katika Delta ya Rufiji kwa kushirikiana na Shirika la Wetland Internationalna taasisi nyingine. Drones zaidi zinategemewa kuletwa nchini muda wowote  kusaidia doria za mwambao wa baharí.

 1. Ujenzi wa Ranger Out-Posts

TFS inajenga ranger outposts katika misitu mbalimbali nchini ili kusogeza usimamizi  karibu na misitu . Kwa mwaka 2018, pekee jumla ya rangers posts 15 zinajengwa katika hifadhi 6 za mazingira asilia pamoja na ofisi za utawala 1 kila hifadhi, aidha ranger posts zaidi ya 12 zinajengwa kwenye misitu kadhaa katika mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma. Hizi zitakamilika mwezi Mei na kazi hii ni endelevu.

 1. Jitihada nyingine
 • Kushirikisha vyombo vingine vya ulinzi katika kusimamia misitu kama SUMA JKT, Polisi nk.
 • Kuwashirikisha wananchi katika maeneo mbalimbali
 • Kurudisha misitu ya Serikali za mitaa iliyoharibika chini ya usimamizi wa serikali kuu (TFS)
 • Kuboresha ufugaji nyuki ili uwe chachu ya uhifadhi, kipato na utalii (Api-tourism, wines etc)..
 • Kutoa mafunzo ya uadilifu pamoja na kuchukua hatua kwa watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma

Mwisho nizishukuru taasisi zote za kimataifa, balozi mbalimbali nchini na asasi za kiraia zinazoshirikiana nasi katika kusimamia rasilimali za misitu nchini. Wengi wamesaidia na wanaendelea kusaidia katika kuandaa matumizi bora ya ardhi katika vijiji maeneo mbalimbali nchini.

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA


 

HABARI YA ZIADA

Tanzania Bara ina eneo la takribani hekta milioni 48 za misitu sawa na asilimia 55 ya eneo lote la nchi kavu lipatalo hekta milioni 88.6. Rasilimali za misitu nchini zinakadiriwa kuchangia moja kwa moja asilimia 3.9 ya pato la Taifa, na nimmuhimili wa sekta nyingine kama nishati, viwanda, kilimo, mifugo, maji, afya, elimu na zinginezo zinazotegemea misitu. Hata hivyo, misitu yetu inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazotishia uharibifu unaopelekea kupungua kwa uwezo wake kutoa huduma za kiekologia na kijamii. Mathalani, katika  miaka ya hivi karibuni kumekuwapo na uvamizi mkubwa wa maeneo ya misitu kwa ajili ya shughuli za kilimo, malisho ya mifugo, uchimbaji wa madini,  makazi na ukataji haramu wa miti kwa ajili ya nishati, mbao na nguzo za ujenzi. Pamoja na shughuli hizi hufanyika katika maeneo mengi ya misitu uvamizi mkubwa umekuwa ukitokea katika misitu iliyoko Kanda ya Magharibi, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Ziwa.

Mbali ya uharibifu kutokea katika misitu ya hifadhi uharibifu mkubwa pia unatokea katika misitu ambayo haijahifadhiwa kisheria katika ardhi za vijiji ukizingatia kuwa takribani asilimia 60 ya eneo la misitu halijahifadhiwa. Hata hivyo, hivi karibuni uharibifu wa Rasilimali Misitu unaongezeka kwa sababu za ukosefu wa umiliki na ukosefu wa mipango shirikishi ya matumizi bora ardhi.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ulianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakala Sura ya 245 na marekebisho yake ya mwaka 2009, kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 269 la Julai 30, 2010. Kuanzishwa kwaTFS kumezingatia pia Sera za Taifa za Misitu Sura 323 na ya Ufugaji Nyuki za 1998 Sura 224; na Sheria za Misitu Na. 14 ya 2002 na Sheria ya Nyuki Na. 15. Vilevile, Wakala uliundwa kwa kuzingatia Programu ya Serikali ya Maboresho katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2000. Programu hii ililenga kuimarisha Idara na Wakala wa Serikali kutoa huduma bora na endelevu, zilizotukuka katika utumishi wa umma. Lengo Kuu la kuanzishwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu ni kuhakikisha uwepo wa usimamizi madhubuti, wenye ufanisi na tija wa rasilimali za misitu na nyuki; kuongeza thamani ya mazao ya misitu na nyuki na kutoa huduma bora kwa umma kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa umma.

TFS imefanya jitihada mbalimbali za kuimarisha usimamizi wa misitu katika nyanja mbalimbali ili kuongeza matokeo chanya ya uhifadhi ambayo ni pamoja na:

 1. Kuainisha na kuhakiki mipaka ambapo eneo la km 238,030.92 limeainishwa na eneo la km 15,237.53 limesafishwa kwa kuweka maboya. Uwekaji maboya umefanyika sambamba na usimikaji mabango kwa ajili ya kutoa tahadhari kwa wananchi kutovamia maeneo hayo; Mpaka sasa jumla ya maboya

21,267 kati ya 22,719 na mabango 8,334 yamewekwa;

 1. Kuzuia wavamizi wa misitu na kuongoa maeneo yaliyoharibiwa;
 2.  Kuendelea kudhibiti makundi makubwa ya mifugo yanayotolewa kwenye mapori na misitu mingine ili yasiingie kwenye maeneo mapya na hifadhi za misitu;
 3. Kuwaelimisha wananchi madhara ya uharibifu wa misitu na mazingira na kuwahimiza kuzingatia kanuni bora za kilimo na kuacha kilimo cha kuhamahama. Kuhimiza mamlaka ya Serikali za mitaa kutayarisha na kutumia mipango bora ya matumizi ya ardhí;
 4. Kuimarisha ushiriki wa wananchi wanaoishi kuzunguka misitu ya hifadhi katika kuhakikisha misitu inalindwa na kuhifadhiwa;
 5. Katika kuongeza wigo wa upatikanaji wa mazao ya misitu, Wakala umeongeza mashamba ya miti ya kupandwa kutoka 19 yenye jumla ya hekta 308,442 hadi 23 yenye jumla ya hekta 444,382.
 6. Kufanya utambuzi/ uhakiki wa vijiji halali na visivyo halali vilivyosajiliwa kimakosa ndani ya hifadhi za misitu. Zoezi hili limefanyika na takribani vijiji 228 vimebainisha kuwa vipo ndani ya hifadhi za misitu ambapo kati ya hivyo, vijiji 157 vina hati ya usajili;
 7.  Kuimarisha usimamizi misitu ikiwa ni pamoja na kuandaa na kusimamia mipango ya usimamizi na uvunaji endelevu wa misitu na kushirikisha wadau katika kuhifadhi misitu. Jumla ya mipango ya usimamizi 39 iliyokamilika imepasishwa kwa ajili ya kutumika kusimamia shughuli za uhifadhi. Aidha,. jumla ya misitu 89 iliandaliwa mipango ya matumizi ambayo 34 imekamilika na kuanza kutumika na mengine 15 ipo katika hatua mbalimbali za kukamilishwa. Mipango ya uvunaji miwili kwenye maeneo ya mataji wazi ya Magamba (Mbozi) na Sibweza (Tanganyika) imeandaliwa.

Sambamba na juhidi hizo TFS na NLUPC wameanza kushirikiana katika kuandaa mipango Shirikishi ya matumizi bora ardhi kwa Vijiji vinavyozunguka Misitu. Vijiji visivyo na mipango na vyenye Migogoro. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania katika mwaka wa fedha 2018/2019, umeendelea kuwezesha vijiji vinavyozunguka misitu ya hifadhi ili kupunguza migogoro kati ya misitu ya hifadhi na vijiji vinavyozunguka hifadhi. Zoezi hili linafanyika kwa njia ya kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuwa na uhakika wa eneo walilo nalo na kuwa na matumizi bayana ya maeneo husika.

Vijiji vya kipaumbele ni kwa vijiji visisivyo na mipango ya matumizi bora ya ardhi, vinavyozunguka misitu ya hifadhi na vyenye migogoro na hifadhi za misitu na visivyo na migogoro. Lengo kubwa likiwa ni kutatua matatizo ambayo yalisababishwa na upungufu wa rasilimali watu, fedha na vitendea kazi na kusababisha misitu mingi kutokufanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara na kusababisha uwepo wa uvamizi kwa shughuli mbalimbali za kibinaadamu kama makazi, Kilimo cha mazao ya muda mfupi na mazao ya kudumu.

Kama nilivyowajulisha awali kuwa zoezi hili linafanywa kwa ushirikiano na Tume ya Taifa ya Usimamizi wa Ardhi, limeanza na mwaka huu wa fedha 2018/2019 ambapo mpaka sasa zoezi limeanza na kanda ya kusini na tayari vijiji 11 vimefanyiwa mipango ya Matumizi bora ya ardhi katika wilaya Nanyumbu, Kilwa, Masasi na Lindi. Aidha, wataalam wanaendelea na zoezi hili kwa kanda zote na zoezi hili litakuwa ni endelevu kadri rasilimali fedha zitakapokuwa zinatengwa kwa kila mwaka wa fedha.

Hivyo basi, Kwa namna ya pekee ninawaomba Waandishi wote wa habari pamoja na vyombo vyote ya habari  kwa umoja wenu, weledi na umahiri wenu katika tasinia za habari mkawe mabalozi wa hili jambo na ninawasihi tuendelee kushirikiana katika kutoa elimu na uelewa sahihi kuhusiana na zoezi hili ambapo Mimi Mtendaji Mkuu wa TFS pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya matumizi ya ardhi tunasaini Mkataba huu wa mashirikiano na Timu ya watalaam inaendelea na zoezi katika Mikoa na Wilaya zote kwa hatua kadri itakavyowezekana.