Uoto Asilia Msitu wa Msaginya ulivyoikosha Kamati ya Bunge

Uhifadhi wa misitu umekuwa ukikumbana na changamoto za aina mbalimbali - kuanzia mabadiliko ya tabiachi ambayo ni matokeo ya uharibifu wa mazingira hadi shughuli za kibinadamu zinazofanyika katika maeneo hayo.

Hata hivyo, nyuma ya changamoto hizo kuna juhudi za aina mbalimbali zinafanyika ili kuifanya misitu istawi, na iweze kulinda uoto wa asili ambao ni chanzo cha maji na uhai wa viumbe.

Msaginya ni msitu wa hifadhi uliopo katika wilaya ya Mlele mkoani Katavi ambao uliwahi kuvamiwa na wananchi walioanzisha shughuli za kilimo na kuathiri uoto wa asili, hali iliyoanza kutishia uoto wa asili.

Hata hivyo, juhudi zilizofanyika kuunusuru, zimeurejeshea hali yake ya uoto wa asili kiasi kwamba sehemu ya baioanuai iliyokuwa imeanza kutoweka, imeanza kurejea kwa kasi.

Msitu wa Msaginya ni sehemu ya mkondo wa mfumo wa misitu iliyopo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambayo inapitiwa na Mto Congo wenye sifa ya pili ya eneo lenye mvua nyingi duniani baada ya msitu wa Amazon uliopo Amerika Kusini.

Awali, msitu huo ulipovamiwa na shughuli za kilimo kutawala, hali iligeuka na kuwa mbaya kwa sababu miti mingi ilikatwa na hata maeneo unamopita palianza kuathirika.

Hata hivyo, licha ya wananchi kuelimishwa, baadhi yao waligoma kuondoka wakisema hawakuwa na maeneo kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao, licha ya kuwapo kwa eneo kubwa la kijiji.

“Lakini zaidi ilikuwa ni suala la kufuata rutuba tu, maana maeneo ya kilimo tunayo - tena makubwa. Lakini eneo lile (la msitu wa Msaginya) lina rutuba maana halikuwahi kulimwa huko nyuma,” anasema Jones, mkazi wa kijiji cha Ikongwe, kata ya Sitalike.

Anasema Serikali wakati ikilifanya eneo hilo kuwa hifadhi iliwaachia eneo kubwa kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao, lakini baadhi yao walikimbilia katika hifadhi kufuata ardhi yenye rutuba ili waendeshe kilimo.

Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Kanda ya Magharibi, Valentino Msusa anasema baada ya kufanya majadiliano mara kadhaa na wananchi waliovamia msitu huo, wengi wao waligoma kuondoka.

Msusa, aliyekuwa akizungumza na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, alisema ilibidi wawaondoe kwa sababu athari zilianza kushika kasi, na hivyo kuwaacha kungeathiri hata mfumo wa ikolojia unaotegemea misitu iliyopo eneo hilo pamoja na ile ya Congo.

“Tunashukuru kwamba baada ya watu kuondoka hali ilibadilika, baadhi ya maeneo yaliyokuwa yameharibiwa sana na miti kukatwa tulipanda mingine na uoto mpya umeanza kurejea na kuimarika,” anasema Msusa.

Anazitaja athari zingine iwapo msitu huo ungeharibiwa na kuendelea kutumika kwa shughuli za kilimo kuwa ni kuharibu shoroba za wanyamapori, ikizingatiwa kwamba uko jirani na Hifadhi ya Taifa ya Katavi eneo lenye wanyama wengi.

“Lakini msitu huu ukiwa katika hali nzuri hata shughuli za ufugaji nyuki zinaweza kufanyika bila tatizo na kama mnavyoona afya ya mimea inaimarika siku hadi siku kwa sasa.”

Kamati ya Bunge

Wakizungumza katika eneo hilo, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii waliunga mkono uhifadhi wa maeneo muhimu yanayotunza uoto wa asili ili kutoharibu mfumo wa maisha ya watu.

Mbunge wa Chambani, Yusuf Salim Hussein alizishauri taasisi na idara za Serikali kutoa elimu zaidi kwa wananchi, ili waweze kujua athari za uharibifu wa maeneo ya hifadhi kwa kuwa wakishajua itakuwa rahisi kwao kuyalinda. “Pamoja na kuwaondoa wananchi waliokuwa wanalima humo, suala ambalo nawaunga mkono, lakini vilevile mjitahidi kuwa mnawapa elimu zaidi. Elimu ikiwakolea wataona tu umuhimu wa kuhifadhi maeneo hayo,” anasema Yusuf.

Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay anasema kuwa, wananchi wakielimishwa ipasavyo watakuwa na uwezo wa kuunda vikundi vyao vya ulinzi kwa ajili ya kuyalinda maeneo hayo.

“Na watajiwekea utaratibu wao na sheria zao zitakazowaongoza. Tuwaelimishe lakini vilevile tuwasaidie maana wao ni muhimu zaidi,” anasema.

Kaimu mwenyekiti wa kamati hiyo, Neema Mgaya anasema watajitahidi kuishauri Serikali kuendelea kusimamia sheria za uhifadhi, huku ikizingatia kwamba wananchi pia wanapaswa kuwa na maeneo kwa ajili ya kuendeshea maisha yao.

Maeneo ya misitu

Rasilimali za misitu nchini zinakadiriwa kuchangia moja kwa moja asilimia 3.9 ya pato la Taifa, ukiachilia mbali shughuli nyingine za sekta mbalimbali kama nishati, viwanda, kilimo, mifugo, maji, afya na elimu zinazotegemea misitu.

Kwa mujibu wa mgawanyiko wa umiliki wa misitu nchini, TFS inasimamia misitu 455 ya Serikali Kuu yenye hekta milioni 15, huku mamlaka ya serikali za mitaa zikisimamia misitu 161 ya hifadhi yenye hekta milioni 2.4 na misitu iliyo katika ardhi za vijiji inayokadiriwa kuwa na eneo la hekta milioni 21.