Ufugaji wa Nyuki Kibiashara na Ubora wa Mazao yake

Karne mbili zilizopita, ufugaji wa nyuki kibiashara ulianza baada ya kuibuka kwa teknolojia za kukabiliana na wadudu hao na kupanuka kwa soko la asali na mazao yake ikiwamo nta inayotumika viwandani.

Licha ya kuwa na zaidi ya miaka 100 ukifanyika, bado biashara ya asali duniani ni fursa kwa wananchi, lakini wengi hawajui kama ipo na imekumbatia utajiri mkubwa.

Tanzania ni nchi ya pili duniani katika uzalishaji asali; zao kuu litokanalo na nyuki ikiwa nyuma ya Ethiopia.

Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), inaratibu shughuli za ufugaji wa nyuki na ushauri wa kibiashara kwa wazalishaji na wauzaji wa asali na mazao yake.

Kalenda ya ufugaji wa nyuki nchini imegawanyika katika misimu minne kulingana na majira kwa mwaka, ambayo hutofautiana kati ya mkoa na mkoa.

Kaimu meneja mawasiliano wa TFS, Tulizo Kilaga anasema katika kila msimu, kazi ya ufugaji wa nyuki hutegemea na kundi la nyuki linahitaji nini na mfugaji afanye nini kuweza kuzalisha mazao ya nyuki.

“Ipo misimu minne ya nyuki kwa mwaka ambayo ni msimu wa njaa, kujijenga kwa nyuki, mtiririko wa asali na msimu wa mavuno kwa mfugaji wa nyuki,” anasema Kilaga.

Msimu wa njaa

Katika msimu huu, huwa ni kiangazi, ukame na mimea        mbalimbali inakuwa imepukutisha maua na majani.

Kalaga anasema matokeo ya kipindi hicho ni chakula cha nyuki kuwa kidogo kwenye mizinga, idadi ya nyuki hupungua mzingani, malkia hupunguza au huacha kutaga mayai, makundi ya nyuki huhama kutafuta sehemu zenye malisho (ubichi) na baadhi ya nyuki hupita kwenye makundi yenye asali ili kuiba.

“Wajibu wa mfugaji nyuki katika msimu huu ni kuchukua tahadhari ya mizinga isivamiwe na maadui wa nyuki mfano sisimizi, nyegere na wengine wanaotaka kuingia ndani ya mzinga,” anasema Kilaga.

Pia, makundi ya nyuki yanayokuwa katika mizinga yanapaswa kukingwa kutokana na jua kali na upepo kwa kuwa maeneo mengi yanakuwa wazi.

“Vilevile kuandaa vifaa vya ufugaji nyuki na kutengeneza mizinga au kuikarabati mibovu. Tunawashauri wafugaji kuyalisha makundi ya nyuki imara kwa asali kama njaa ni kali,” anasema.

Msimu wa kujijenga

Akizungumzia msimu wa nyuki kujijenga, kaimu meneja Misitu wa Wilaya ya Manyoni, Juma Ismail anasema hicho ni kipindi ambacho mvua za awali zinakuwa zimeanza na mimea inachanua kwa wingi.

Anasema makundi ya nyuki hupita kutafuta makazi na pia huzungukazunguka kwenye mzinga na sehemu nyingine.

“Wakati huu ndiyo ule ambao nyuki hujenga masenga ya asali, huzaliana ili kuongeza idadi kwenye mzinga, yapo mengine hupita kutafuta makazi na yapo ambayo huhama kwenye mizinga endapo kuna maadui au mzinga kuwa mbovu

Anasema katika kipindi hicho ni wajibu wa mfugaji kufanya ukaguzi wa mizinga, kusafisha na kuanika mizinga isiyo na nyuki, kutafuta makundi ya nyuki ili kuwezesha mzinga kuwa na nyuki kwa kutundika mizinga ya kukamatia makundi sehemu ambayo nyuki hupitapita.

Mtiririko wa asali

Katika kipindi hiki; miti na vichaka vinakuwa vimechanua maua huwa ni mengi na nyuki wanatembelea maua kukusanya mbochi (majimaji matamu yanayotengenezwa na maua) na chavua.

Ismail  anasema  katika wakati huu, ukipita karibu na mimea yenye maua utasikia sauti za nyuki ambao hukusanya mbochi na kuibadilisha kuwa asali, lakini maadui wa nyuki mfano siafu, sisimizi na wengineo huongezeka jirani na kundi la nyuki.

 Mavuno

Akizungumzia msimu wa mavuno kwa mfugaji, Kilaga anasema ni kipindi ambacho maua ya mimea yamepungua na kuanza kutoa mbegu ama matunda. Kiangazi pia ndiyo huwa kinaanza.

Anasema wakati huu nyuki huongeza ulinzi nje ya mzinga na huwa wakali ili kulinda asali yao, kwa baadhi ya mizinga nyuki hujikusanya nje.

Pia, anasema katika kipindi hicho nyuki hupunguza kupitapita kwenye maua au kuhama.