Resources » News and Events

TFS YAPONGEZWA KWA KUCHANGIA MAENDELEO

Mufindi. Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Mhe. David William ameupongeza uongozi wa Shamba la Miti Saohill kwa kuhakikisha shamba hilo linaendelea kuchangia katika ukuaji wa uchumi, kuwaongezea wananchi kipato na kuongeza fursa za ajira.

William aliyasema hayo Mufindi jana mara baada ya kuupokea ugeni wa Wakuu wa Wilaya ya Namtumbo, Nyasa na Songea za mkoani Ruvuma walioambatana na wadau wa Shamba la Miti Mpepo lililopo mkoani humo kwenye ziara ya kikazi katika Shamba la Miti Saohill. Alisema, katika kipindi cha miezi kumi (Julai 2018 hadi Mei 2019) shamba hilo limeweza kukusanya zaidi ya Milioni 700 katika zao la utomvu huku lilikusanya zaidi ya Bilioni 47 katika uvunaji wa miti kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Kaimu Meneja wa Shamba la Miti Saohill, Daniel Silima anasema katika kipindi cha miaka kumi (2008 – 2019) shamba hilo limeweza kukusanya zaidi ya bilioni 319 huku lilikusanya bilioni 6 kama mrabaha wa mauzo ya miti (CESS)  kwa Halmashauri za Wilaya ya Mufindi, Mji wa Mafinga na Kilombero.

Mkuu wa Wilaya ya Nyansa Mhe. Isabela Chilumba ambae pia ndie kiongozi wa msafara huo anasema waliamua kufanya ziara ya kujifunza shambani hapo kutokana na mafanikio yake katika sekta ya misitu na ufugaji nyuki. “Tumejifunza mengi lakini kubwa ni namna uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kupitia shamba hili unavyoendelea kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba Sekta ya Maliasili inazidi kuimarika ili kuyafanya mazao yatokanayo na maliasili hususan misitu na nyuki yanaendelea kuchangia katika ukuaji wa uchumi, kuwaongezea wananchi kipato na kuongeza fursa za ajira, “  anasema Chilumba.

Katika ziara hiyo wageni hao walipata fursa ya kuona shughuli za ufugaji nyuki na kiwanda kidogo cha kuchakata asali, kuona shamba, kutembelea bustani ya Miti, kuona shuguli za ugemwaji wa utomvu na kutembelea Viwanda vya kuchakata mazao ya misitu ili kujionea kazi mbalimbali zinazofangika katika shamba la Saohill na jinsi Msitu huo ulivyo na faida kwa vijiji vinavyozunguka.