NAIBU WAZIRI KANYASU AITAKA TFS KUSHIRIKIANA NA WADAU KUNUSURU MISITU

Dodoma. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Costantine Kanyasu , amewataka watendaji wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kushirikiana na mamlaka za Serikali za mitaa, sekta binafsi na jamii katika kusimamia misitu.

Mhe. Kanyasu ametoa kauli hiyo leo Septemba 25, 2019 wakati akifungua kikao maalumu cha utendaji ambacho kimewakutanisha pamoja viongozi wa TFS kuanzia makao makuu hadi katika ngazi ya wilaya jijini hapa.

Akizungumza leo Jumanne Septemba 25, 2019 wakati wa ufunguzi wa kikao maalumu cha utendaji kilichowakutanisha pamoja viongozi wa TFS kuanzia makao makuu hadi katika ngazi ya wilaya, Mhe. Kanyasu amesema rasilimali za misitu zinategemewa kwa kiasi kibwa na jamii lakini usimamizi wake unahusisha mamlaka za Serikali za mitaa, sekta binafsi na jamii kwa jumla.

“Mtawanyiko huu wa usimamizi unatoa changamoto mbalimbali ambazo zinaonesha umuhimu wa kushirikiana kiutendaji na kisera. Mathalani ushirikiano wa Maafisa misitu (DFOs) walioko katika halmashauri zetu na ninyi mameneja wa Wilaya (DFMs) ni jambo ambalo wakati wote linapaswa kutiliwa mkazo.

“Wote mnasimamia misitu kama rasilimali ya taifa hakuna haja ya kutafuta nani aliye mkubwa wa mwenzie. Ni lazima DFMs na DFOs muheshimu mgawanyo wa majukumu yenu kama yalivyobainishwa katika mwongozo wa usimamizi wa misitu nchini, “anasema Mhe. Kanyasu.

Aidha amesema Serikali ya awamo ya tano chini ya Mheshimiwa Rais Dr. John Joseph Magufuli imeweka msisitizo mkubwa katika uhifadhi na maendeleo ya viwanda. Msukumo ambao unalenga kuleta ukombozi wa uchumi kwa wananchi kupitia ajira za viwandani na kuongeza thamani ya mazao.

Mhe. Kanyasu anasema ni vizuri jitihada za uhifadhi zikatangulia na kuungwa mkono na wananchi wote ili viwanda vipate kushamiri. “Na hii inamaanisha lazima kila mtu kwa nafasi yake atimize wajibu wake. Hapa kwenye misitu wote wenye dhamana wasimamie rasilimali misitu kwa weledi na umahiri wa hali ya juu,”.

Naibu Waziri huyo anasisitiza kuwa bila hifadhi thabiti ya misitu viwanda vitashindwa kufanya kazi yake sawasawa kutokana na uhusiano wa misitu na upatikanaji wa maji/mvua, uhusiano wa misitu na mabadiliko ya tabia ya nchi, uhusiano wa upatikanaji wa maji na uzalishaji wa umeme unaotumika viwandani na majumbani, na uhusiano wa mvua na maendeleo ya sekta ya kilimo na mifugo nchini.

Kamishna Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo anasema TFS imejengea mtandao wa usimamizi wa misitu katika maeneo yote nchini. Hivyo kwa kukutana mameneja wa kanda, mameneja wa mashamba, wakuu wa vitengo na Mameneja wote wa Misitu wa Wilaya (DFMs) leo kutasaidia kuleta pamoja fursa za kujadili mafanikio na changamoto za sekta ya misitu.

“Tunategemea kikao kazi hiki chenye wajumbe 210 kitatumika kama hatua muhimu ya kufikia malengo ya usimamizi wa misitu kwa kukumbushana wajibu wa kila mtumishi katika eneo lake kupokea changamoto zinazojitokeza field na kuweka mkakati wa namna ya kuimarisha utendaji wetu katika ngazi zote za wakala ili kufikia malengo yetu na ya serikali kwa jumla,” anasema Prof Silayo