MWENYEKITI WA BODI TFS AIPONGEZA TFS KWA UTENDAJI ULIOTUKUKA

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara Maliasili na Utalii kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Brigedia Generali Mbaraka Mkeremy amewapongeza waahasibu na watumishi wa TFS kwa kuchagiza TFS kupata Hati Safi za Ukaguzi.

Akizungumza katika kikao na Watumishi wa Kanda ya Nyanda ya Juu Kusini jijini Mbeya jana, Brigedia Generali Mkeremy alisema licha ya TFS kuwa na changamoto nyingi katika utekelezaji wa majukumu yale watendaji wake wameweza kufanya kazi kwa weredi na hata kufanikiwa kupata hati safi kwa mara ya kwanza.

“Najua taasisi hii ina changamoto nyingi lakini niwapongeze kwa namna mlivyojituma na hata kuweza kupata hati safi ya ukaguzi, hati hii ni matokeo ya uwajibikaji katika makusanyo na matumizi. Nimeelezwa kuwa TFS pia ilivuka malengo ya makusanyo, na imefanikiwa kupunguza malalamiko na kutokuwapo migogoro baina ya watumishi na hayo ni kiashiria cha mafanikio ya taasisi,” Brigedia Generali Mkeremy alisema.

Hii ni mara ya kwanza kwa Brigedia Generali Mkeremy kuzungumza na watumishi wa kada tofauti wa TFS tangu Waziri wa Maliasili na Utalii Dk.Hamisi Kigwangalla aizuindue Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) jijini Mwanza na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali Machi 9,2019.

Brigedia Jenerali Mkeremi alisema kukabiliana na baadhi ya changamoto hususan ujangiri TFS imeamua kuingia kwenye Jeshi Usu ili kuhakikisha uhifadhi endelevu wa misitu nchini.

Kamishna Mhifadhi wa Misitu, Prof. Dos Santos Silayo aliwataka watumishi kuendelea kushirikiana katatika kutatua changamoto za kiutumishi na kiutendaji huku akitanabaisha kuwa mabadiliko ya Jeshi Usu yataenda sambamba na TFS kutoka kwenye Wakala na kuwa Mamlaka kamili.