Mtendaji TFS ataja Mikakati ya Mapato ya Serikali

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeweka mikakati kadhaa Kuhakikisha misitu inaingiza mapato ya kutosha kupitia huduma za utalii sambamba na kuuza mazao ya misitu.

Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuvitangaza vivutio vya utalii vya ikolojia vilivyopo kwenye misitu ya mazingira asilia iliyopo chini ya taasisi hiyo.

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa nane wa baraza la wafanyakazi wa TFS lililofanyika Morogoro, Profesa Silayo amesema aina hiyo ya utalii na biashara ya mazao ya misitu na nyuki ni nguzo ya utendaji wao wa kazi.

Akitoa mfano wa uvunaji wa utomvu wa miti inayokaribia kuvunwa katika shamba la Sao Hill, amesema bidhaa hiyo inahitaji kufanyiwa utafiti na kuangalia uwezekano wa kuongeza uzalishaji wake.

Amesema katika eneo hilo pia upo uwezekano wa kuongeza uzalishaji wa gundi kutoka katika miti ya migunga, zao linalotarajiwa kuingiza fedha nyingi siku za usoni.

Profesa Silayo amesema ni jukumu la watumishi wa taasisi hiyo kuongeza jitihada za utendaji wao ili kuhakikisha lengo hilo linatimia na kuleta matokeo chanya.

Pia amegusia suala la udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu na nyuki, pamoja na kushindwa kuimarisha huduma katika vivutio vya utalii.

 “Haya ni maeneo ambayo inabidi tujipange vizuri zaidi kuyatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kuondoa kero na kutoa huduma bora kwa umma,” amesema mtendaji huyo.

“Endapo tutaimarisha maeneo haya, itasaidia kuongeza tija katika jukumu letu la ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kuongeza mauzo ya nje na fedha za kigeni kupitia huduma za utalii na uuzaji wa mazao ya nyuki.”

Pia amesisitiza kuhusu nidhamu kwa watumishi na kuwataka kila mmoja kutimiza wajibu wake huku wakijiepusha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya kazi, na kusisitiza kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kukiuka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) wa TFS, Francis Kiondo amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma kwa kila mtumishi pindi anapotekeleza majukumu yake.

Kikao hicho kimehudhuriwa na zaidi ya wajumbe 120 kutoka TFS makao makuu, mashamba ya miti na wawakilishi kutoka ofisi za wakala huo za kanda.