MIPANGO YA MATUMIZI BORA YA ARDHI KWA VIJIJI VINAVYOZUIZUNGUKA HIFADHI YA SERIKALI KUU WAJA

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania -TFS imeendesha kikao kati yake na ofisi ya Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi – NLUPC kwa ajili ya kuhakikisha kunakuwepo na mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa vijiji 120 vinavyozunguka misitu ya Hifadhi ya Serikali Kuu.

Kikao kazi hicho kimefanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa TFS uliopo Jengo la Mpingo jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Mtendaji Mkuu wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho cha siku moja Professa Silayo alisema kikao hicho kinalenga kumaliza changamoto ya kuhifadhi misitu nchini.

“Mpaka sasa zaidi 60% ya misitu iliyopo nchini haijahifadhiwa na lengo letu ni kuhakikisha misitu hiyo inahifadhiwa. Hivyo ninakitaka kikosi kazi hiki kihakikishe lengo hili linafikiwa kwa kuweka mikakati ya kitaaaluma kwa kuzingatia wakati uliopo,” alisema Professa Silayo. 

Professa Silayo anasema hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayoielekeza Serikali Kutatua migogoro ya mipaka kati ya wananchi na maeneo ya jirani na hifadhi kwa kushirikisha wadau katika kuhakiki mipaka ya maeneo ya hifadhi kwa kuweka alama za kudumu; kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi; na kuzingatia utawala wa Sheria katika kusimamia rasilimali za maliasili.
Mtendaji huyo anaongeza kuwa uharibifu wa misitu nchini ni mkubwa katika maeneo ambayo vijiji vimeanzishwa ndani ya misitu bila kufuata sheria na TFS imeendelea kuzuia upanuzi zaidi wa vijiji hivyo, na hadi sasa kuna vijiji 228 vinavyofahamika na miji kadhaa. 

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi Dkt. Stephen Nindi anasema kuwa ofisi yake iko tayari kutoa utaalam huo ili kunusuru rasilimali za nchi wakati wowote kwa faida ya Watanzania.

Kikosi kazi hicho kinahusisha wataalam kutoka TFS na NLUPC kimekaaa pamoja kuweka mikakati ya namna bora ya kufanya kazi hiyo hiyo leo kwa kukabidhiana orodha ya misitu ya hifadhi yenye migogoro kwa kanda zote saba za TFS ambazo ni Kanda ya Mashariki, Kaskazini, Kati, Kusini, Nyanda za juu Kusini, Ziwa na Magharibi, na kupitia hatua za kawaida za kupanga ni kwa namna gani matumizi bora ya ardhi yatawezeshwa kwa vijiji hivyo.