Mkurugenzi wa Rasilimali za Misitu Akipanda Mti Siku ya Maadhimisho Aprili,01.2019

Watanzania wametakiwa kuwa na utamaduni wa kupanda na kutunza miti, ili kujiondoa kwenye athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Rasilimali za Misitu na Nyuki Zawadi Mbwambo wakati wa maadhimisho ya siku ya upandaji miti.

Mbwambo ambaye aliongoza wadau mbalimbali kupanda miti katika eneo la Kilongawima pembezoni mwa mto Ndumbwi unaopeleka maji katika Bahari ya Hindi  jijini Dar es Salaam amesema mabadiliko ya sasa ya hali ya hewa ni matokeo ya uharibifu wa mazingira.

Amesema, “Hata mvua zinavyokuwa bila mpangilio ni matokeo ya uharibifu huo, tumeona ipo haja ya kurekebisha hilo na tunafanya kwa kupanda miti,”

“Mwaka huu tumeona tusifanye sherehe za kitaifa kinachofanyika ni kuadhimishwa kikanda kila maeneo watu wanapanda miti na hapa tulipo ni eneo la TFS linalosimamiwa na Kanda ya Mashariki,”

Amesema kwa mwaka huu TFS imeamua kupanda miti katika maeneo ambayo yameathiriwa zaidi na lengo la zoezi hilo ni kuyarudishia kwenye uoto wake wa asili.

Katika eneo la Kilongawima ambalo ni ukanda wa pwani jumla ya miti 1000 imepandwa ikiwemo mivinje na mikoko.

Kwa upande wake Meneja wa Misitu wa Wilaya ya Kinondoni Dotto Ndumbikwa alitoa wito kwa jamii inayozunguka kushirikiana na TFS kuitunza na kuilinda miti hiyo iliyopandwa, na kuahidi kuimarisha doria ya pamoja, na kuwachukulia hatua wale wote watakaofanya uharibifu wa miti kwa kuingiza mifugo kama vile ng'ombe na mbuzi.

  • Chanzo cha kukithiri joto, kutonyesha mvua chatajwa;

Watanzania wametakiwa kuwa na utamaduni wa kupanda na kutunza miti, ili kujiondoa kwenye athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira

Imeelezwa kukithiri kwa joto na mvua kuchelewa kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi yanayochochewa na uharibifu mkubwa wa mazingira.

Kufutia hilo Watanzania wametakiwa kuwa na utamaduni wa kupanda miti na kuhifadhi misitu ili kuwa na uhakika wa mvua na hewa safi.

Wito huo umetolewa leo Jumatatu Aprili 1, 2019 na Mkurugenzi wa Rasilimali za Misitu na Nyuki wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Zawadi Mbwambo wakati wa maadhimisho ya siku ya upandaji miti.

Mbwambo ambaye ameongoza watumishi wa taasisi hiyo kupanda miti katika eneo la Kilongawima jijini Dar es Salaam amesema mabadiliko ya sasa ya hali ya hewa ni matokeo ya uharibifu wa mazingira.

Amesema hata kukithiri kwa joto katika baadhi ya maeneo nchini kunatokana na uharibifu huo unaohusisha ukataji wa miti.

“Hata mvua zinavyokuwa bila mpangilio ni matokeo ya uharibifu huo, tumeona ipo haja ya kurekebisha hilo na tunafanya kwa kupanda miti. Tungekuwa na miti ya kutosha tusingefikia hatua ya viongozi wa dini kuomba mvua.”

“Mwaka huu tumeona tusifanye sherehe za kitaifa kinachofanyika ni kuadhimishwa kikanda na ngazi ya mikoa kila maeneo watu wanapanda miti,” amesema.

Amesema kwa mwaka huu TFS imeamua kupanda miti katika maeneo ambayo yameathiriwa zaidi na lengo la zoezi hilo ni kuyarudishia kwenye uoto wake wa asili.

Katika eneo la Kilongawima ambalo ni ukanda wa Pwani jumla ya miti 1,000 imepandwa ikiwemo mivinje na mikoko.

Mwakilishi wa taasisi ya Great Hope inayohamasisha vijana kupanda miti, Noela Mahuvi amesema ni muhimu kwa suala la upandaji miti kupewa kipaumbele na jamii nzima.

“Hilo suala tunapaswa kulifanya la kitaifa, kila mmoja aguswe kwenye nafsi yake apande mti kwa lengo la kutunza mazingira,” amesema.

“Sisi tunajipanga kuwa na kampeni itakayohamasisha wanafunzi wa sekondari kupanda miti angalau kila mwanafunzi apande mti mmoja kwa mwaka,” amesema.