Resources » News and Events

Jeshi Lashirikiana na TFS kupanda Miti

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikina na Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kilichopo Kunduchi wamepanda miti kando kando ya mto Tegeta.

Katika zoezi  hilo lililofanyika asubuhi ya leo Katibu wa chuo hicho Kanali Furahisha Ntahena aliwaongoza wanafunzi hao wanajeshi kupanda miti.

Kanali Ntahena amesema wamefikia uamuzi huo kwa lengo la kukabiliana na athari za mazingira ambazo zimeanza kuonekana kutokana na uharibifu uliofanyika.

Amesema jeshi limeona ipo haja ya kushiriki kwenye kampeni ya upandaji miti kwa kwa kuwa athari za mazingira zinapotokea zinaikumba jamii nzima.

“ Athari za mazingira zikitokea hazichagui, sasa kutokana na uharibifu ambao wote tumeuona tuna kila sababu ya kushiriki kwenye kampeni hii ya upandaji miti,”

“Tunapanda kando kando ya mto Tegeta lakini hatuishii hapa tutapanda pia kwenye maeneo yetu na vilevile tutawapa miti mingine wanajeshi wakapande kwenye makazi yao,”

Katika zoezi hilo jumla ya miti 2000 ilipandwa kwenye mto huo ambao umeathiriwa na shughuli za kibinadamu.

Kwa upande wake Meneja wa TFS wilaya ya Kinondoni Dotto Ndumbikwa ameziomba taasisi na watu binafsi kushiriki kwenye kampeni ya upandaji miti ili kutunza mazingira.

“Ikitokea la kutoa kutokana na athari za uharibifu wa mazingira tutakaoathirika ni wote, hivyo ni muhimu kila mmoja kwenye nafasi yake akatunza mazingira,”

Ndumbikwa ameeleza kuwa katika wilaya yake ya Kinondoni uharibifu wa mazingira ni mkubwa na unachangiwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo uvamizi katika maeneo ya mito.