Resources » News and Events

TFS yakamata magogo yaliyovunwa kinyume cha utaratibu-Rufiji

Slipa 1356 zinazotokana na miti ya mtondoro,  mkuruti na mgunga chuma zenye ujazo wa cubic mita 267.39 na thamani ya Tshs  61,064,150 zimezuiliwa kwa sababu hazikufuata taratibu za uvunaji na usafirishaji kama zinavyoainishwa kwenye sheria ya misitu.

Aidha Jumla ya magogo 288 aina ya mkuruti,  mitikii na mnangu yenye ujazo wa cubic meter 73.477 na thamani ya Tshs 13,862,912 yamezuiliwa kwa sababu hizohizo. Hayo yametokea eneo la ikwiriri na nyamwage baada ya kampeni maalum iliyofanyika katika maeneo hayo ya wilaya ya Rufiji ambapo magogo yasiyogongwa nyundo,  yenye alama ya mshale yalibainika kusafirishwa kwa vibali visivyo halali vya kusafirishia.

Katika hatua nyingine mvunaji saidi Majungu ambaye alikuwa ameruhusiwa kuvuna cbm 20 tu kihalali alikuwa amevuna cbm 127  na amediriki kusafirisha mbao zisizo na kibali kutoka msituni mpaka eneo la kuchakata.

Naye mchakataji mwenye kampuni ya Mhavile alishindwa  kujibu maswali ya mkurugenzi wa matumizi ya rasilimali za misitu  alipomtaka aseme kiwanda chake kina uwezo wa kuchakata cubic mita ngapi na kwa muda gani badala yake  alisema hakuwa akiweka rekodi kwa sababu hazikuwahi kuhitajika kwa muda mrefu na kwa kuwa sasa zinahitajika atazirekodi

Wakati huohuo mmiliki wa kampuni ya Miko alisema alipokea amri kutoka Kwa mkuu wa wilaya aliyeondoka Bw.  Nurdin Babu ambaye sasa ni mkuu wa wilaya ya sengerema kwamba amsaidie kuchakata magogo ili apate mbao za kutengeneza  madawati hata hivyo magogo hayo yaliyokuja na amri ya mkuu wa wilaya hayakufuata taratibuza uvunaji wala uchakataji

Mkurugenzi wa matumizi ya rasilimali za misitu wakala wa Huduma za misitu Bwana Mohamed Kilongo ameagiza magogo na slipa zote ambazo zimebainika hazikufuata taratibu wahusika wapigwe faini na kisha kuachiwa kiasi ambacho wanastahili kama mgao wao na kinachobaki kizuiliwe serikali itafanyia maamuzi matumizi yake

Aidha amesema kuna haja ya kuimarisha ulinzi kwani kumekuwa na magogo yanayovunwa nje ya eneo kinyume cha utaratibu kisha kuletwa kufichwa kwenye misitu iliyopo Rufiji kwa ajili ya kusafirisha kinyume cha utaratibu.